Tangazo

November 27, 2015

MWILI WA MAWAZO KUAGWA KITAIFA KATIKA UWANJA WA FURAHISHA JIJINI MWANZA

Mkutano wa Naibu Katibu Mkuu Chadema Salum Mwalimu na Wanahabari Jijini Mwanza hii leo.
Na:Binagi Media Group
Mwili wa aliekuwa Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo Chadema Mkoa wa Geita Marehemu Alphonce Mawazo, kesho unatarajiwa kuagwa Jijini Mwanza kabla ya kusafirisha kwenda Mkoani humo kwa ajili ya Mazishi.

Kaimu Katibu Mkuu wa Chadema Salum Mwalimu, amesema Marehemu Mawazo ataagwa Kitaifa kwa taratibu za chama hicho, katika uwanja wa Furahisha Jijini Mwanza.

Amesema ratiba hiyo itatanguliwa na ratiba ya kifamilia ya kuuaga mwili huo, ambayo itafanyika asubuhi Nyegezi Jijini Mwanza ambako ni nyumbani kwa Mchungaji Charles Lugiko ambae ni baba mdogo wa Marehemu Mawazo hiyo ikiwa ni baada ya mwili wake kutolewa katika Hospitali ya Rufaa Bugando ulikohifadhiwa.

Mwalimu amebainisha kwamba mwili huo utasafirishwa hiyo kesho kwenda Mkoani Geita kuanzia majira ya saa nane mchana ambapo wakazi wa Mkoa huo pia watapata fursa ya kuuagwa kesho kutwa jumapili.

Ameeleza kwamba kuanzia majira ya saa mbili asubuhi, shughuli za kuuaga mwili huo zitafanyika Kimkoa katika Uwanja wa Magereza Mjini Geita na baadae kusafirisha kwenda Katoro ambapo wakazi wa Jimbo lake la Busanda watapata fursa ya kuuaga mwili huo.

Mwalimu ametanabaisha kwamba, baada ya shughuli zote hizo kukamilika, mazishi ya Marehemu Mawazo yanatarajiwa kufanyika siku ya Jumatatu katika Kijiji cha Chikobe Jimbo la Busanda Mkoani Geita.

Shughuli zote hizo zinatarajiwa kuongozwa na Mwenyekiti wa Chadema Taifa Freeman Mbowe, Viongozi waandamizi wa Chama hicho akiwemo Frederick Sumaye, aliekuwa mgombea urais wa Ukawa Edward Lowasa, wabunge pamoja na makada wa Chadema.

Ratiba za Mazishi ya Marehemu Mawazo ambae aliuawa Novemba 14 mwaka huu na watu wasiojulikana, zimejiri baada ya Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza jana kuondoa zuio la Jeshi la Polisi Mkoani Mwanza, lililokuwa zinazuia mwili huo kuagwa Jijini Mwanza kutokana na hofu ya kiusalama pamoja na uwepo wa mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu ambapo zuio hilo liliondolewa katika kesi iliyofunguliwa na baba mlezi wa Mawazo, Mchungaji Charles Lugiko baada mvutano mkali wa siku nne mahakamani hapo.
BONYEZA PLAY HAPA CHINI KUSIKILIZA
Naibu Katibu Mkuu Chadema, Salum Mwalimu akionyesha kibali kilichotolewa na Manispaa ya Ilemela ili kuruhusu ibada ya kumuaga Marehemu Mawazo Kufanyika kesho katika Uwanja wa Furahisha
Mkutano wa Naibu Katibu Mkuu Chadema Salum Mwalimu na Wanahabari Jijini Mwanza hii leo (hawapo pichani).
Kushoto ni Ezekiel Wenje na Kulia ni Grace Kihwelu ambae ni Mbunge Viti Maalumu Chadema Mkoani Kilimanjaro
Singo Kigaila Benson ambae ni Mkurugenzi wa Mafunzo Chadema (Kushoto) akiwa na Peter Mekele ambae ni Mwenyekiti Chadema Kanda ya Ziwa Victoria (Kulia)
Husna Amri Said ambae ni Mwenyekiti BAWACHA Wilayani Geita
Viongozi na Makada wa Chadema
Mkutano wa kutoa ratiba za kuuaga mwili wa Marehemu Mawazo kwa wanahabari Jijini Mwanza hii leo
Wanahabari

No comments: