Tangazo

December 15, 2014

MAMA KIKWETE AWAPA TAHADHARI VIJANA KUTOKUBALI KUDANGANYWA NA KUTUMIWA KUFANYA VURUGU

Na Anna Nkinda – Maelezo, Lindi
 
 Vijana wa wilaya ya Lindi mjini wametahadharishwa kutokubali kudanganywa na kutumiwa kufanya  vurugu ambazo zinaharibu vitu vichache walivyonavyo na  kwa kufanya hivyo wanarudisha nyuma maendeleo yao.

Tahadhari hiyo imetolewa jana na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM)  kupitia wilaya hiyo  Mama Salma Kikwete wakati akiwanadi wagombea wa chama hicho kwenye mkutano wa kufunga kampeni za uchaguzi wa Wenyeviti na Wajumbe wa Serikali za mitaa uliofanyika katika Kata ya Makonde.

Mama Kikwete ambaye ni Mke wa Rais Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete alisema ni vyema vijana wakaelewa historia ya nchi yao na kujua lipi jema na baya kwani kuna baadhi ya wanasiasa wanawashawishi ili wafanye vurugu kwa madai kuwa hakuna maendeleo yoyote yaliyopatikana jambo ambalo siyo kweli.

“Hao wanaowadanganya nyinyi mfanye vurugu na kuharibu vile vichache mlivyonavyo eti kwa kuwa maisha yenu hayajaimarika kwao hawafanyi hivyo, kwao kuna maendeleo na ninyi mnazidi kujirudisha nyuma kimaendeleo. Msikubali  mkoa wetu uwe sehemu ya majaribio na kutumika kwa manufaa yao”.

Kama wangekuwa  wanawapenda na kutaka kuwasaidia ili muendelee wangewajengea hata shule ambazo zingewafanya vijana na watoto wetu wasome, hapo hakuna kipingamizi kwani Elimu ni mkombozi wa maisha na elimu inaleta maendeleo”, alisema Mama Kikwete.

MNEC huyo alisema Serikali makini ni lazima ijali maisha ya watu wake, kwa kutambua hilo Serikali ya CCM imeimarisha miundo mbinu kwa kujenga barabara za lami,  shule ili watoto wasome na kuimarisha huduma za afya ikiwa ni pamoja na kujenga Hospitali na  vituo vya afya na kuhakikisha wahudumu wa afya wanaongezeka.

Alisema, “Maisha bora kwa kila mtanzania siyo Chama kinapita nyumba kwa nyumba kugawa pesa bali ni kwa kuboresha miundombinu, kukiwa na shule watoto watasoma, kukiwa na barabara nzuri wananchi wasafirisha mazao yao, kukiwa na huduma bora za afya wananchi watatibiwa haya yakifanikiwa  maisha ya mtu mmoja mmoja yataimarika”.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Lindi Mjini Muksini Rafii alisema katika uchaguzi huo ndani ya wilaya hiyo wagombea za nafasi za wajumbe 147 na wenyeviti saba wamepita bila kupingwa.

Kwenye mkutano huo mwanachama mmoja aliyejulikana kwa jina la Raphael Mahuna  kutoka Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA)  ambaye alikuwa ni mgombea wa nafasi ya Mwenyekiti wa mtaa wa National Housing kwa tiketi ya chama hicho na mwanachama mmoja  kutoka Chama cha Wananchi (CUF) walijiunga na Chama Cha Mapinduzi.

Mahuna alisema ameamua kwa hiari yake mwenyewe bila ya kulazimishwa kujiunga na CCM kwani alipokuwa anagombea nafasi ya Mwenyekiti wa mtaa wa National Housing alishindwa kufanya kampeni kwa kuwa alikosa  wajumbe wa kumuunga mkono.

Katika uchaguzi wa Serikali za mitaa, vijiji na vitongoji mkoani  Lindi wagombea wa Chama Cha Mapinduzi katika vitongoji 600, vijiji 87 na mitaa nane wamepita  bila kupingwa.

No comments: