Tangazo

October 24, 2014

KAIRUKI: Serikali kuendelea kuiwezesha Tume Opresheni Tokomeza

 Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Angellah Kairuki (MB) akibadilishana mawazo na Mwenyekiti wa Tume ya Rais ya Uchunguzi wa Operesheni Tokomeza Jaji Kiongozi Mstaafu Hamis Amir Msumi (kushoto) na Wajumbe wengine wa Tume hiyo, Majaji Wastaafu Stephen Ihema (kulia) na Vincent Lyimo ofisini kwake jijini Dar es Salaam leo (Oktoba 22, 2014)
xxxxxxxxxxxxxxxx
Na Mwandishi wetu

Serikali imeahidi kuendelea kuiwezesha na kuipa ushirikiano Tume ya Rais ya Uchunguzi wa Operesheni Tokomeza ili iendelee kutekeleza na hatimaye kukamilisha majukumu yake kama ilivyokusudiwa.

Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Mheshimiwa Angellah Jasmine Kairuki amesema hayo jijini Dar es Salaam leo (Jumatano, Oktoba 22, 2014) wakati akizungumza na Wajumbe wa Tume hiyo waliomtembelea ofisini kwake ili kubadilishana mawazo.

“Serikali itaendelea kuwapa ushirikiano na kuwawezesha ili mtekeleze majukumu yenu kama ilivyokusudiwa,” amesema Naibu Waziri katika mkutano huo uliohudhuriwa na Mwenyekiti wa Tume Jaji Kiongozi Mstaafu Hamis Amir Msumi na Wajumbe wengine Jaji Mstaafu Stephen Ihema, Jaji Mstaafu Vincent Lyimo na Katibu wa Tume hiyo Wakili Fredrick Manyanda.

Ahadi ya Naibu Waziri Kairuki ilifuatia kauli ya Mwenyekiti wa Tume hiyo kuwa Tume yake imekuwa ikipata ushirikiano wa kutosha kutoka kwa wananchi na Serikali tangu ilipoteuliwa tarehe 1 Mei mwaka huu.

“Tunashukuru kwa ushirikiano tunaoupata kutoka Serikalini,” amesema Jaji Msumi na kufafanua kuwa viongozi wa Serikali wa wilaya na mikoa wametoa ushirikiano mzuri kwa Tume yake katika awamu ya kwanza ya kukusanya taarifa na malalamiko.

Jaji Msumi amesema kuwa katika awamu hiyo iliyofanyika katika mikoa ya Kigoma, Katavi, Rukwa na Mbeya wananchi na viongozi wa Serikali katika maeneo hayo walitoa ushirikiano mkubwa.

“Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi wa Halamashauri walitupa ushirikiano wa kutosha na wananchi walikuwa na shauku kubwa ya kukutana na Tume,” amesema Jaji Msumi alipokuwa akizungumzia awamu ya kwanza ya ziara ya Tume yake iliyofanyika kuanzia tarehe 17 Septemba, 2014 hadi 6 Oktoba mwaka huu.

Jaji Msumi pia amemweleza Naibu Waziri kuwa Tume yake inatarajia kuanza awamu ya pili ya kutembelea mikoa sita ya Kanda ya Ziwa kuanzia kesho (Alhamisi, Oktoba 23, 2014) hadi tarehe 18 Novemba mwaka huu ili kukusanya taarifa na malalamiko katika kuhusu Operesheni Tokomeza. Mikoa itakayotemebelea na Tume hiyo ni Kagera, Geita, Shinyanga, Simiyu na Mara.

Rais Jakaya Kikwete, kwa mujibu wa Kifungu cha 3 cha Sheria ya Uchunguzi Sura ya 32, aliunda Tume ya Uchunguzi (Commission of Inquiry) kuhusu vitendo vilivyotokana na uendeshaji wa Operesheni Tokomeza tarehe 1 Mei mwaka huu.

No comments: