Tangazo

September 1, 2014

Wanawake wataka umuhimu wa uwepo wa masuala ya jinsia katika Katiba

Mwenyekiti wa Umoja wa Wabunge Wanawake Tanzania (TWPG), Mhe. Anna Abdallah akifungua Semina iliyoandaliwa na Umoja huo kwa kushirikiana na Mtandao wa Wanawake na Katiba kwaajili ya Wajumbe wa Bunge Maalum kuhusu masuala ya Jinsia na Katiba iliyofanyika 30 Agosti, 2014 kwenye Ukumbi wa Bunge wa Pius Msekwa Mjini Dodoma.
Na Benedict Liwenga, Maelezo-Dodoma.

UMOJA wa Wabunge Wanawake Tanzania (TWPG) kwa kushirikiana na Mtandao wa Wanawake na Katiba wamezungumzia juu ya umuhimu wa uwepo wa masuala ya jinsia katika Katiba Mpya na masuala muhimu ya jinsia ya kuzingatiwa katika katiba.

Wito huo umetolewa 30 Agosti, 2014 wakati wa Semina iliyoandaliwa na Umoja huo wakishirikiana na Mtandao wa Wanawake na Katiba ili kutambua usawa na haki za wanawake ili kuleta hali ya usawa kati ya wanaume na wanawake katika maamuzi, majukumu ya kazi, umiliki wa rasilimali pamoja na haki zao kwa ujumla.

Akitoa mada wakati wa semina hiyo, Mjumbe wa Mtandao wa Wanawake na Katiba Bi. Usu Mallya amesema kuwa suala la msingi wa usawa wa kijinsia ni muhimu kuwekwa katika Katiba Mpya na baadaye kuwepo na uwajibikaji wake kwani kwa kufanya hivyo kutaipatia nchi katiba yenye mlengo wa kijinsia.

Bi. Mallya ameongeza kuwa wanawake wengi nchini hawapati fursa ya usawa wa kijinsia katika nyanja mbalimbali licha ya Tanzania kuwa kinara wa kutoa wanawake vinara ambao wamewahi kushika nyazifa mbalimbali na wengine bado wakiendelea kushika nafasi hizo za juu hapa nchini.

“Utafiti unaonyesha kuwa, asilimia 5% ya wanawake nchini ndiyo wanaomiliki ardhi, asilimia 39% ya wanawake hao hao hawapati elimu, pia utafiti unaonyesha kuwa asilimia 40.3% ya wanawake walioko kwenye ajira wapo katika sekta isiyo rasmi, wakati asilimia 10% ya Maprofesa wanawake ndiyo tunayo hapa nchini”. Alisema Bi. Mallya

Aidha, Bi. Mallya amezitaja changamoto mbalimbali wanazokabiliana na wanawake wengi nchini kuhusiana na usawa wa kijinsia na haki zao pamoja na haki za watoto huku akitoa taarifa za utafiti zinazoonyesha kuwa mzigo wa kazi wa asilimia 66% ya wanawake wanafanya kazi zisizo na kipato na asilimia 44% ya wanawake walioolewa katika ndoa zao wamefanyiwa ukatili wa kijinsia.

Naye Mwenyekiti wa Women Fund Tanzania ambaye pia ni Mjumbe wa Mtandao wa Wanawake na Katiba, Profesa Ruth Meena amezungumzia juu ya masuala ya umuhimu wa jinsia ya kuzingatiwa katika Katiba Mpya huku akisisitiza juu ya usawa wa uongozi katika ngazi zote uwe hamsini kwa hamsini na uwepo wa chombo maalum kitakachozingatia haki za wanawake.

Profesa Meena ameongeza kuwa kuna umuhimu wa Katiba Mpya iweze kulinda haki za watoto kwa kutoruhusu ndoa za utotoni, hivyo kuwekwe sheria zitakazo mlinda mtoto dhidi ya ndoa hizo mpaka mtoto anapotimiza umri wa miaka (18) kumi na nane.

“Suala la umri wa mtoto wa kike kuolewa iwe ni miaka kumi na nane, na mtu atakayeoa mtoto chini ya miaka kumi na nane awe amebaka”. alishauri Profesa Meena.

Aidha, Profesa Meena amegusia kuhusiana na suala zima la haki ya uzazi salama kwa wanawake pindi wanapojifungua liweze kupewa kipaumbele kwa kujali usalama wa maisha ya mama na mtoto na suala hilo, lisiwe hukumu ya kifo kwao.

“Iwe ni haki yetu ya uhai tunapofanya kazi ya kuongeza kizazi cha Tanzania, wanawake wapewe usalama wa uzazi wanapozaa pasipokuwa na kugugumizi, hivyo kuzaa kusiwe hukumu ya kifo kwa watoto wetu”. alisema Profesa Meena.

Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba, Mhe. Samia Suluhu Hassan amewatia moyo wanawake kwa kuwa na umoja wa kudai haki zao za usawa wa jinsia na amesisitiza juu ya ushirikiano kati ya wanaume na wanawake katika jamii.

Mhe. Samia, amewaasa wanaume wasiwe na tabia ya kuwadharau wanawake katika masuala mbalimbali yakiwemo uongozi ama kuwapa talaka pindi wanawake wapatapo fursa ya uongozi.

Naye Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Mhe. Sophia Simba ameitaka jamii kuwekea mkazo suala la elimu ya uzazi ianze kutolewa kuanzia elimu ya msingi ili watoto waweze kuwa na uelewa wa kutosha pindi wanapokuwa na ametoa msisitizo juu ya usawa kati wanawake na wanaume wa hamsini kwa hamsini katika masuala yote katika jamii.

Shirika la UN Women ndilo mwezeshaji wa Semina hiyo kwaajili ya Umoja wa Wabunge Wanawake Tanzania na Mtandao wa Wanawake na Katiba kwa ajili ya Wajumbe wa Bunge Maalum kuhusu masuala ya jinsia na Katiba, ambapo ni mara ya kwanza kwa semina kama hii kufanyika nchini Tanzania jambo ambalo limewavutia wajumbe wengi waliohudhuria wakiwemo wanaume na wanawake.

No comments: