Tangazo

September 11, 2014

WAJAWAZITO WAKIJIFUNGUA KATIKA MAZINGIRA SALAMA VIFO VYAO VITAPUNGUA - SALMA KIKWETE

Mama Salma Kikwete
Na Anna Nkinda – Maelezo

Ili kuhakikisha vifo vya kina mama wajawazito vinapungua ni lazima wajifungue katika mazingira salama huku kukiwa na upatikanaji wa kutosha wa vifaa tiba.

Hayo yamesemwa jana na Mke wa Rais Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete Mama Salma Kikwete wakati akiongea na viongozi wa Bohari ya Dawa (MSD) iliyopo Keko Jijini Dar es Salaam.

Mama Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) alitembelea makao makuu ya MSD kwa ajili ya kuangalia vifaa tiba ikiwa ni pamoja na vifaa vya kujifungulia  kina mama wajawazito.

Alisema kama mama atajifungua katika mazingira salama nchi itaweza kuvuka malengo ya milinia ya kupunguza vifo vya kina mama wajawazito ambavyo kwa sasa vimepungua kutoka 452 kwa kila vizazi hai 100000 hadi kufikia 432 kwa kila vizazi hai 100000 jambo ambalo litasababisha maisha ya mama kuwa bora. 


“Moja ya kazi zinazofanywa na taasisi ya WAMA ni kuboresha afya ya mama na mtoto hapa nchini, katika hili tunatoa vifaa tiba vikiwemo vitanda vya kujifungulia kina mama wajawazito katika Hospitali, vituo vya Afya na Zahanati  ili kuhakikisha kina mama wanajifungua katika mazingira salama” .

Wakati wa ziara ya Rais Kikwete  mkoani Morogoro niliahidi kutoa vitanda vya kujifungulia ili kina mama waweze kujifungua salama, nimekuja hapa na nimejionea vitanda vizuri na vya kisasa vya kujifungulia pamoja na vifaa vingine ambavyo vinatumika kwa mama mjamzito naahidi nitawapelekea vifaa hivyo”, alisema Mama Kikwete.

Aidha Mama Kikwete pia aliwataka viongozi hao kuongeza juhudi  katika utendaji wao wa kazi  ya kuokoa maisha ya binadamu na kuhakikisha dawa wanazozipokea zinafika kwa mlaji kwa wakati kwani kama zitafika kwa wakati vifo vitapungua.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa MSD Cosmas Mwaifwani alisema tangu mwaka wa fedha uliopita wameanza kupeleka dawa na vifaa tiba moja kwa moja katika ngazi ya vituo vya afya na kuvifikisha kwa mlaji nia ikiwa ni kufikisha huduma hii kwa mlengwa kwa ubora unaotakiwa na kwa wakati.

“Dhina ya MSD ni  kuwezesha upatikanaji wa vifaa tiba vyenye ubora kwa bei naafuu kwa watanzania wote, ndiyo maana tunafika Tanzania nzima na hata kule ambako kuna ugumu wa kufika zinaangaliwa njia mbadala za kufika huko”. 

Hivi sasa tunaweza kusimama na kuizungumzia dhina hii bila wasiwasi kwani kwa sasa tafiti zinaonyesha kuwa upatikanaji wa dawa na vifaa tiba umeongezeka kutoka asilimia 45 hadi kufikia asilimia 85”, alisema Mwaifwani.

Alisema pamoja na kwamba MSD inashughulikia Hospital, Zahanati na Vituo vya afya vya Serikali na taasisi zilizoidhinishwa na wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii bado ipo tayari kutoa huduma kwa  makundi mengine ambayo yanatuma maombi kwa ajili ya kununua vifaa tiba kwa matumizi ya wananchi.

Mwaifwani alisema, “Pale ambapo kundi la watu ama mtu binafsi anapohitaji vifaa tiba kwa ajili ya matumizi ya wananchi na vifaa hivyo vikiwepo MSD, hatutakuwa na hiyana ya kutompatia huduma hiyo kwani tumedhamiria kuokoa maisha ya watanzania”.

Bohari ya Dawa ni moja ya Idara inayojitegemea chini ya Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii inajiendsha chini ya Bodi ya wadhamini yenye majukumu makuu matatu ambayo ni kununua, kuhifadhi na kusambaza dawa, vifaa tiba na vitendanishi vya maabara kwa Hospitali za Serikali na zile zilizoidhinishwa na wizara. 

No comments: